Mahakama maalum zitapunguza mlundikano wa wafungwa
Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na mazingira, haki za binadamu na jinsia (Envirocare).
Uanzishwaji wa Mahakama maalumu (zinazohamishika) na watoa msaada wa
kisheria katika maeneo ya magereza, kutapunguza mlundikano wa wafungwa.
Ripoti ya hali ya mahabusu za watoto na watu wazima kwenye mikoa mitano ya Tanzania, inaeleza hayo katika
utafiti uliofanywa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha
na mazingira, haki za binadamu na jinsia (Envirocare).
Mkurugenzi wa Envirocare, Loyce Lema, alisema ripoti hiyo imependekeza
Mahakama zinazohamishika, kutokana na mlundikano wa mahabusi, wengi
wakiwa wana kesi ndogondogo.
“Katika magereza 16 na mahabusi za
watoto nne, tumegundua wengi wako huko kwa kuwa hawana uelewa wa
sheria, wana kesi ndogo ndogo hawastahili kuwapo humo,” alisema.
Mratibu wa mradi huo, ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Envirocare,
Catherine Jerome, alisema ulianza Septemba, mwaka jana, walitembelea
magereza katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na
Kilimanjaro.
Alisema lengo la mradi ni kuishauri serikali
namna bora ya kupunguza mlundikano wa mahabusi mojawapo ikiwa ni kuwa na
wasaidizi wa masuala ya kisheria watakaowaelekeza mahabusi jinsi ya
kupata dhamana na haki nyinginezo.
Jerome alisema wametoa
mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria 88, wawili wenye cheti cha sheria
kutoka miongoni mwa maafisa wa gereza na wawili kutoka kwenye jamii
jirani na gereza.
Mwasilishaji wa ripoti hiyo kwa wanasheria,
watendaji wa Jeshi la Polisi na Magereza katika mkutano wa pamoja
kuijadili uliofanyika jijini Dar es Salaam, ambaye pia ni Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Issai Seng’enge, alisema mahabusi 2,896
walihojiwa.
Alisema katika magereza saba kuna wafungwa na
mahabusi wengi kuliko uwezo wa mahakama na wengi hawana uelewa wa
masuala ya sheria kwani asilimia 69.42 wana elimu ya msingi na asilimia
84.37 wanatoka kwenye familia za kipato cha chini.
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kennedy Gastorn, alisema kwa Tanzania
Bara kuna magereza 122 zenye uwezo wa kubeba watu 29,400, lakini
waliopo ni 32,000 na asilimia 51 ni wanasubiri hatima ya kesi zao.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment