Hayo yalielezwa jana na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Ignas Kitusi, wakati akizungumza na NIPASHE, juu ya uwepo wa sheria ya kuwawezesha Mahakimu hao kufanya kazi katika Mahakama hizo.
Alisema Mahakimu hao waliajiriwa mwanzoni mwa mwaka jana na walipelekwa kwenye mafunzo ya uhakimu kwa wiki moja katika chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Lushoto mkoani Tanga.
Alisema baada ya kuhitimu walisambazwa kwenye Mahakama mbalimbali nchini na walikuwa wanajifunza kazi kutokana na kutokuwepo kwa sheria ya kuwaruhusu kufanyakazi kwenye Mahakama hizo.
“Kazi ya uhakimu ni lazima mtu ajifunze, walikwenda kwenye vituo vya kazi kujifunza kazi na mwezi Aprili, mwaka huu, sheria ilipitishwa na kuwawezesha kufanya kazi…kabla ya hapo hawakuwahi kuamua kesi yoyote,” alisema.
Kitusi alisema kati yao 10 walihama na kwenda kwenye maeneo mengine ya utumishi wa umma.
Aidha, NIPASHE ilivyotaka kujua iwapo Mawakili wataanza kufanya kazi katika mahakama hizo, alisema elimu ya Hakimu haibadili hadhi ya Mahakama hivyo mawakili hawatatumika katika mahakama hizo.
Wakati wa kikao cha Bunge, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, akiwasilisha Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2012/13, alisema mafunzo ya awali (Induction Course) kwa ajili ya Mahakimu Wakazi wapya 290 waliokuwa wameajiriwa kufanya kazi katika Mahakama za Mwanzo sehemu mbalimbali nchini yameshafanyika.
CHANZO ( NIPASHE - Salome Kitomary )
No comments:
Post a Comment