NILIWAHI kuandika kwamba rasimu ya Katiba mpya ni kubwa na inahitaji kupitiwa taratibu ili kuielewa vema. Nilipanga kuijadili sehemu kwa sehemu katika makala hizi lakini kwa sababu ya matukio mbalimbali niliweka kando kidogo kazi hiyo na kuyajadili yale ambayo niliona yalikuwa na haraka na umuhimu kwa wakati husika.
Leo nataka kuiangalia sehemu ya kumi ya rasimu ya Katiba yetu ambayo inahusika na Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lengo langu ni kuangalia upungufu wa eneo hili katika rasimu yetu ili kuipa maboresho zaidi kwa mustakabali wa mhimili huu adhimu kwa haki za Watanzania.
Jambo kubwa na la haraka ninaliona katika sehemu hii ya rasimu ya Katiba inayozungumzia Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni madaraka makubwa ya rais katika mhimili huu. Kilio hiki si kigeni. Ni kilio kilichopo hata katika Katiba inayotumika sasa.
Ukiitazama kwa ujumla rasimu hii unaweza kusema kama Katiba mpya itapita bila mabadiliko katika sehemu hii, Mahakama inaweza kujikuta katika kwapa la Serikali. Ni kama imebinywa zaidi kuliko ilivyo kwa Bunge. Ukisoma sura hii ya kumi ya rasimu ya Katiba unaweza kupata picha kwamba mhimili huu wa dola ni dhaifu kuliko mihimili ile mingine miwili ya dola.
Kwanza kazi ya kumteua jaji mkuu chini ya Ibara ya 151 ya rasimu hii ya Katiba inafanywa na rais kisha kuthibitishwa na Bunge. Hapa kuna maswali mengi ambayo yanatufanya tuone kama uhuru wa Mahakama unaweza kuwa shakani. Jambo la kwanza rais ambaye anatokana na chama anafungwa na chama chake.
Hivyo kama itatokea rais akawa hana msimamo thabiti wa kizalendo, tunaweza kujikuta tukimpata jaji mkuu aliyeteuliwa si kwa kigezo cha uwezo wake bali mahaba yake kwa chama kinachotawala. Ni kweli kwamba rais anafanya uteuzi huo kutokana na majina yanayopendekezwa kwake na Tume ya Utumishi wa Mahakama. Lakini hapa napo ni kama mazingaombwe.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba Tume hiyo ya Utumishi wa Mahakama nayo inateuliwa na rais chini ya ibara ya 172. Hivyo ni kusema kwamba rais anateua jina la jaji mkuu kutokana na majina aliyopewa na watu aliowateua.
Madaraka ya rais ni makubwa mno kwa maana kwamba ikiwa ana uwezo wa kuteua tume ya kuchagua majina atakayotumia kuteua Jaji Mkuu, basi ina maana kwamba rais ana uwezo wa kushawishi upatikanaji wa jaji mkuu. Hili si jambo lenye afya.
Lakini pia ukitazama ibara hii ya 151 utaona pia kwamba baada ya uteuzi wa rais, Bunge linatakiwa kumthibitisha jaji mkuu. Hapa ndipo linapokuja swali, hivi mhimili wa Mahakama ni mdogo kuliko ule wa Bunge? Kwa nini mkuu wa mhimili mmoja athibitishwe na wajumbe wa mhimili mwingine?
Wapo watakaorukia kusema hizo ni njia za kudhibiti madaraka yasitumiwe vibaya. (Checks and balances). Ikiwa hivyo ndivyo kwa nini wabunge nao wasithibitishwe na mahakama baada ya kuchaguliwa? Au walau wale wa kuteuliwa na rais kwa nini wasithibitishwe na Mahakama katika uteuzi wao? Au baada ya waziri mkuu kuteuliwa kwa nini asithibitishwe pia na Mahakama?
Swali la msingi hapa ni ikiwa itatokea Bunge linalomuidhinisha jaji mkuu lina wingi wa wabunge kutoka chama kimoja, je, uhuru wa jaji huyu hauwezi kuyumbishwa na wanasiasa? Na hapa tatizo liko zaidi katika mchakato mzima, kwamba huenda tukamkosa jaji anayefaa kwa sababu ya itikadi za kisiasa.
Kwa maana kwamba kama kuna jaji ambaye wabunge wa chama chenye wingi bungeni wanadhani hafai kwa maslahi ya chama chao wanaweza kumkataa bila kujali vigezo vya ubora wake. Lakini hata baada ya uchaguzi unaweza kumpata jaji mkuu anayedhani ana wajibu wa kurudisha fadhila kwa waliomuidhinisha.
Hata kama jaji huyo mkuu hatakuwa na upendeleo lakini akafika kutoa maamuzi yanayoonekana kukibeba chama kitakachokuwa madarakani, ile kauli maarufu ya kwamba si tu haki itendeke bali ionekane inatendeka, itakuwa imepigwa ngwara. Huu ni udhaifu wa kufanyia kazi katika rasimu hii.
Pengine mapendekezo ya kurekebisha hali hii ingekuwa kwanza kumuondoa rais kuwa mteuzi wa jaji mkuu. Badala yake Tume ya Utumishi ya Mahakama ambayo nayo uteuzi wake unapaswa kubadilishwa, iwe na jukumu hilo. Pengine ili tumpate jaji mkuu bora ni vizuri nafasi hiyo inapokuwa wazi ikatangazwa na wale wote wenye sifa na vigezo wakaomba kazi hiyo.
Mchakato uwe wa uwazi na waombaji wafanyiwe usahili na jopo la wataalamu. Pia isiwe kuthibitishwa na Bunge bali yeyote mwenye sababu za msingi za kumpinga mtu kupewa wadhifa huo aruhuhsiwe kuziweka sababu zake hadharani na Tume ya Utumishi wa Mahakama ikizipima kwa vigezo vitakavyowekwa iwe na uwezo wa kukubali au kumuondoa mtu kuwania nafasi hiyo. Huu pia ungekuwa utaratibu mwafaka kwa uteuzi wa majaji wote wa Mahakama za Rufani na Mahakama ya Juu.
Mamlaka yaliyopitiliza ya rais katika uteuzi wa majaji pia unaonekana katika Ibara ya 153 (3) ya rasimu hii ya Katiba. Katika Ibara hii rais anapewa mamlaka ya kutengua sifa ya muda anaotakiwa mteule kuwa na sifa husika na kisha kumpa ujaji mhusika.
Hapa rais anapewa rungu la kutengua sifa za mtu kuwa jaji, na mtu huyo kuteuliwa kuwa jaji hata kama hana sifa stahili kwa kipindi kilichotajwa kikatiba. Haya ni mamlaka makubwa mno. Ibara hii inasema kwamba kwa kushauriana na Tume ya Utumishi ya Mahakama.
Angalia neno lililotumika ni “kushauriana”. Katika kushauriana si lazima wakubaliane. Inatosha tu yeye kuwaambia wajumbe wa tume kwamba yeye anataka kuteua jaji ambaye hana sifa zinazostahili kwa muda husika, na ikiwa tume itakubali au itakataa, rais bado anakuwa na uwezo wa kuendelea na uteuzi wake.
Tofauti hii ya uchaguzi wa maneno inaonekana tena katika Ibara ya 166(3) ambayo inampa rais uwezo wa kuteua kaimu jaji wa Mahakama ya Rufaa ikiwa “ataridhika” na ushauri wa jaji mkuu. Hapa bado nguvu iko kwa rais kuridhika na ushauri wa Jaji Mkuu. Na haielezwi ni mambo gani yatakayomfanya aridhike au asiridhike.
Je, pendekezo la jaji ambaye ameangusha serikali katika hukumu zake unaweza kumfanya rais asiridhike na ushari wa jaji mkuu? Ni madaraka mapana sana hayo na hayajawekewa vizingiti. Matashi na akili binafsi ya rais (yakiwa mazuri) ndiyo salama yetu kama ibara hii itabaki ilivyo.
Mambo mengine yanayonifanya nione kwamba rais bado anakuwa na mamlaka makubwa mno katika mhimili huu wa mahakama ni ukweli kwamba katika rasimu hii ya Katiba, rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua si tu Tume ya Utumishi ya Mahakama bali pia kuteua Msajili wa Mahakama na Mtendaji Mkuu wa Mahakama. Kwa kutazama hayo machache ninapata shaka kama uhuru wa mahakama utakuwa vile ambavyo wengi tungependa.
Chanzo cha Habari ( Tanzania Daina na Juvenalis Ngowi )
No comments:
Post a Comment